Skip to main content

Sura Ya Tatu

3. Jinsi Dorothy Alivyomuokoa Kifukuzakunguru
Dorothy alipoachwa peke yake alianza kuhisi njaa. Basi akaenda kabatini akajikatia kipande cha mkate kisha akapaka siagi. Alimpa Toto pia mkate, akachukua ndoo na akaenda mtoni kuteka maji. Toto alikimbia mitini ambapo aliwaona ndege na akaanza kuwabwekea. Dorothy alimfuata na hapo mitini aliweza kuona matunda matamu ambayo alichukua kidogo ili ale kama staftahi.
Akarudi tena kwenye nyumba na baada ya kutuliza kiu kwa maji matamu ya mto alianza kupanga safari yake ya kuelekea Jiji la Zumaride.
Dorothy alikuwa na rinda moja nyingine tu lakini hilo lilikuwa safi na lilikuwa limeanikwa kwenye msumari kando ya kitanda chake. Nalo hili lilikuwa la madoadoa ya rangi ya samawati na nyeupe. Lakini rangi ya buluu ilikuwa imepungua umaridadi wake baada ya kuoshwa mara nyingi, lakini bado ilikuwa nguo nzuri sana. Msichana alinawa kwa uangalifu na kuivalia nguo hio ya bafia yenye madoafoa.Akavalia kofia yake ya kujikinga kutokana na jua iliyokuwa rangi ya waridi. Akachukua kijikapu akajaza mkate kutoka kwa kabati kisha akafunika kwa kitambaa cheupe juu. Alipoangalia viatu vyake aliona ya kuwa vilikuwa vimezeeka na kuchakaa.
" Hivi viatu kweli havitafaa kwa safari ndefu." Dorothy alimwambia Toto. Toto alimwangalia usoni Dorothy kwa macho yake meusi akatingiza mkia wake kumuashiria ya kuwa alielewa alichokua akimaanisha.
Hapo basi Dorothy alitazama na kuona viatu vya fedha vilivyokuwa vya mchawi wa mashariki.
"Vyaweza kunitosha kweli,'' alimwambia Toto." Viatu hivi vinafaa kweli kwa safari ndefu kwa sababu haviwezi kuharibika.
Alivitoa viatu vyake vilivyokuwa vimezeeka na kuvalia viatu hivyo vya fedha ambavyo vilimtosha vizuri; kana kwamba vilitengenezewa yeye tu.
Mwishowe akachukua kikapu chake. " Hebu kuja Toto," alisema," Tutakwenda Jiji la Zumaridi na kumuuliza Au,mganga mkuu, tutakavyorudi Kansas tena."
Alifunga mlango kwa kifunguo na kukiweka kifunguo mfukoni mwa rinda lake. Akaanza safari yake, Toto akifuatilia kwa mwendo wa aste aste.
Kulikuwako na barabara nyingi alizoziona lakini ilimchukua muda mfupi na hatimaye aliweza kuipata barabara iliyokuwa imetengenezwa na matofali ya rangi ya manjano. Safari yake ikaanza rasmi akaanza kuifuata barabara akielekea Jiji la Zumaridi, viatu vyake vya fedha vikitoa sauti nzuri alipotembea barabarani.
Ndege waliimba kila mahali kwa sauti nzuri huku jua likiwa limewaka kwa nguvu. Dorothy hakuwa na masikitiko kama unavyodhani msichana mdogo angehisi baada ya kubebwa na kimbuga na kuwekwa katika nchi asiyoifahamu.
Alipokuwa akitembea alishangazwa kuona nchi ilivyokuwa maridadi kila mahali alipotazama.Kando ya barabara kulikuweko na sera maridadi iliyokuwa imepakwa rangi ya buluu.Kwa umbali aliona shamba zilikuwa na mazao mazuri ya nafaka mbali mbali na pia aina nyingi za mboga. Munchkini walikuwa wakulima hodari sana.
Mara kwa mara alipopita kando ya nyumba ya mmojawapo wa Munchkini,wenyeji walitoka na kumuinamia kwa sababu walijua ni kwa sababu yake mchawi mwovu wa mashariki aliuawa na kuwakomboa watu wote. Nyumba walizoishi Munchkini zilikuwa za kushangaza mno. Muundo wake ulikuwa wa duara, paa lilifanana kama nusu tanga. Nyumba zote zilikuwa zimepakwa rangi ya samawati.
Ilipofika jioni Dorothy alianza kuwa na uchovu mwingi baada ya kutembea kwa muda mrefu. Dorothy alianza kuwaza atakapolala usiku uingiapo. Alifika kwenye nyumba moja iliyokuwa kubwa kuliko zingine. Nje ya nyumba hiyo kulikuwa na wanaume na wanawake waliokuwa wakicheza densi.Wanamuziki walionekana wakicheza muziki kwa ushupavu na walipaaza sauti sana.Pia karibu nao Dorothy aliliona jimeza lilokuwa limejaa matunda, punje, mikate, keki na vitu vingi kochokocho vya kula.
Watu hawa walimkaribisha Dorothy kwa moyo mkunjufu aje ale nao na apate mahala pa kulala usiku huo.Nyumba hii ilikuwa ya Munchkini tajiri sana nchi yote, na alikuwa amewakaribisha marafiki wake waje kwa sherehe ya kuachiliwa huru kwao kutoka kwa mchawi mwovu.
Dorothy alikula na akashiba sana. Mwenye nyumba alimpakulia kile alichotaka yeye mwenyewe.Jina la Munchkini tajiri lilikuwa Boku.Walikaaa kwenye sofa na kuwatazama watu wakicheza densi.
"Yaonekana ya kuwa wewe ni mchawi mwenye nguvu nyingi sana." Boku alisema baada ya kuviona viatu vyake Dorothy vyenye rangi ya fedha.
"Mbona wasema hivyo?" aliuliza msichana.
"Kwa sababu una viatu vya fedha na ulimuua mchawi mwovu.Halikadhalika nguo yako ni nyeupe na ni wachawi peke yake huvaa nguo nyeupe."
"Nguo yangu ni buluu na ina madoadoa meupe," alisema Dorothy,huku akinyorosha nguo lake.
"Umefanya vyema kuvalia hivyo," alisema Boku."Buluu ni rangi ya Munchkini na nyeupe ni rangi ya wachawi.Basi tunajua wewe ni mchawi mwema."
Dorothy alishindwa asememe nini.Yeye alijua ya kuwa hakuwa mchawi alikuwa tu msichana aliyebebwa na kimbuga kutoka mbali na kuletwa hapa hata ingawa watu wote walimdhania kuwa mchawi.
Baada ya kuchoka kutazama densi,mwenye nyumba alimwonyesha chumba chake cha kulala.Chumba hiki kilikuwa na kitanda maridadi mno.Matandiko yalikuwa ya rangi ya buluu.Dorothy alilala fofofo.Toto alilala kwenye mkeka uliokuwa wenye rangi ya buluu kando ya kitanda chake Dorothy.
Dorothy alikula kiamsha kinywa kikubwa.Baadaye alimuona mtoto mchanga Munchkini,aliyekuwa akicheza na Toto.Mtoto huyu alimchekesha sana Dorothy alivyovuta mkia wake Toto na ucheshi wake.Watu hawa walimchunguza sana Toto kwa sababu hawakuwa wamewahi kumuona mbwa.
"Jiji la Zumaridi liko umbali gani?" alimuuliza msichana.
''Sijui mimi," alimjibu Dorothy kwa kuogopa."Sijawahi kwenda huko.Watu wameonelea kutomkaribia Au isipokuwa kama una mambo muhimu naye.Njia ya kuelekea Jiji la Zumaridi ni ndefu na itakuchukua siku nyingi kufika.Nchi unayopita kwa sasa ni nzuri lakini utapita penye hatari huko mbele kabla ufike mwisho wa safari yako."
Jambo hili lilimsikitisha Dorothy kidogo, lakini alijua tu ni Au aliyeweza kumsaidia.Basi akaamua kwa ushujaa kuendelea na kutorudi nyuma.
Aliwaaga marafiki wake na kuuanza safari yake kwenye njia ya matofali yenye rangi ya manjano.Baada ya kutembea maili kadha aliona apumzike basi akapanda juu ya sera na kuketi chini.Kulikuwa na shamba la mahindi kubwa mbali kidogo na sera.Kwa umbali aliliona Kifukuzakunguru, lilokuwa limewekwa juu kwa kijiti kirefu kufukuza ndege wasile mahindi yaliokuwa yameiva.
Dorothy alilitazama Kifukuzakunguru kwa mawazo akilini.Kichwa chake kilikuwa kimetengenezwa kwa gunia lililojazwa nyasi, macho yake, pua, na mdomo yalikuwa yamechorwa kwa rangi kuonyesha sura yake.Kofia kukuu, iliyokuwa na muumbo wa pia, ya rangi ya buluu, kama ya munchkini ilikuwa imewekwa kichwani mwake.Mwili wake wote uliokuwa na nguo za rangi ya buluu ulikuwa umejazwa nyasi.Kwenye miguu yake alivalishwa viatu vilivyokuwa vimechakaa vya rangi ya buluu kama alivyoviona na Munchkini wengine nchini kwote.Kitu hiki kilikuwa kimeinuliwa juu, juu ya mimea ya mahindi kwa kijiti kirefu kilichokuwa kimewekwa mgongoni mwake.
Dorothy alipokuwa akiitizama uso wa kifukuzakunguru uliokuwa umepakwa rangi alishangazwa kuona jicho lake moja likimkonyezea.Alidhani pengine alikuwa amekosea mwanzoni, kwa sababu nyumbani Kansas vifukuza kunguru kweli hawajawahi kukonyeza macho. Kitu hiki sasa likaanza kutingiza kichwa chake kwa kumuita.Akashuka kutoka kwenye sera na kuanza kutembea kuelekea upande wake.Toto alikimbia na kukizunguka zunguka kijiti huku akibweka.
"Hujambo," alisema Kifukuzakunguru, kwa sauti yenye ambayo haikuwa laini.
"Umezungumza"? aliuliza msichana, kwa mshangao.
"Ndio," alimjibu Kifukuzakunguru. "Hujambo?"
"Sijambo, ahsante," Dorothy alijibu kwa heshima. "Hujambo ?"
"Nina maumivu," alisema Kifukuzakunguru kwa tabasamu."Nimechoshwa sana kukaa hapa usiku na mchana kuwafukuza kunguru."
"Huwezi shuka?" aliuliza Dorothy.
"Hapana kwani kijiti hiki kimewekwa mgongoni mwangu na hakiwezi kutoka.Kama unaweza kukitoa nitakushukuru sana."
Dorothy aliinua mikono yake na kukitoa Kifukuzakunguru kutoka kwa kijiti hicho.Hakikuwa na uzito kwani kilikuwa kimejazwa nyasi tu.
"Ashanti sana," alisema Kifukuzakunguru alipowekwa chini. "Najisikia kama mtu mpya"
Dorothy alishangazwa sana na haya aliyoyaona kwa sababu hakuterejea kumuona mtu aliyekuwa amejazwa nyasi, akizungumza, akiona, akimwinamia na akitembea kando yake.
"Wewe ni nani?" aliuliza Kifukuzakunguru baada ya kujinyoosha."Na waelekea wapi?"
"Jina langu ni Dorothy," alisema Dorothy."Naelekea Jiji la zumaridi kumuomba Au Mkuu anirudishe Kansas."
"Jiji la Zumaride liko wapi?" aliuliza. "Na Au ni nani?"
"Kwani humjui? aliuliza kwa mshangao.
"Kwa uhakika la.Sijui chochote.Unaona mimi nimejazwa tu nyasi sina akili hata," alisema kwa huzuni.
"Ooo!" alisema Dorothy."Pole sana"
"Unadhani ," aliuliza, "Nikienda Jiji la Zumaridi na wewe, kuwa Au atanipa akili?"
"Siwezi kujua," alisema, "Lakini waweza kuja nami ukipenda.Ikiwa Au atakupa akili au hatakupa hutakuwa umepoteza chochote."
"Huo ni ukweli,"alisema."Wajua," aliendelea,"sijali ikiwa miguu yangu na mwili umejazwa nyasi, kwa sababu siwezi umia.Yeyote akinikanyaga kwa mguu au kunidunga kwa pini haijalishi kwa sababu sitaihisi.Lakini sitaki watu waniite mpumbavu.Kichwa changu kikiwa kimejazwa nyasi badala ya akili kama lako nitawezaje kujua chochote?"
"Naelewa unayosema," alisema msichana akimwonea huruma sana. "Ukiandamana nami nitamwomba Au akufanyie yote awezayo."
"Ahsante," alijibu kwa shukrani.
Walirudi barabarani.Dorothy alimsaidia kuruka sera na wakaanza safari yao kwenye njia ya matofali yenye rangi ya manjano wakielekea Jiji la Zumaridi.
Toto hakupendezwa na huyu mgeni mpya.Alinusanusa kana kwamba kulikuwa na panya ndani yake kwenye nyasi na mara kwa mara alimgurumia Kifukuzakunguru.
"Usimjali Toto," alimwambia Dorothy rafiki wake mpya. "Hawezi kuuma."
"Mimi siogopi," alimjibu Kifukuzakunguru."Hawezi kuiumiza nyasi.Wacha nikubebee kapu lako.Haitakuwa mzingo kwa sababu sichoki.''Nikuambie siri," aliendelea, akitembea.
"Kuna kitu moja tu duniani ambalo mimi huogopa."
"Na ni nini hicho?" aliuliza Dorothy."Mkulima Munchkini aliyekuumba?"
"La," alijibu Kifukuzakunguru. "Kiberiti kilichowashwa."

Comments

Popular posts from this blog

Swahili translation of the Wonderful Wizard of Oz

Hii ni tafsiri ya kitabu cha L. Frank Baum, The Wonderful Wizard of Oz. Jina lake baada ya kufikiri na kuchunguza maana ya Oz nimeona katika kiswahili ,"Mganga Ajabu Wa Au." Oz lilitokana na ufupisho wa neno Ounce  ambacho ni kipimo cha dhahabu, Kwa ksiwahili ni Aunsi nami nikafupisha likawa Au, ambayo imenipa Mganga Au. I will publish a chapter by chapter of the whole book. Copyright 2011

Mganga Ajabu Wa Au, sura ya kwanza

MGANGA AJABU WA AU 1. Kimbuga Dorothy aliishi katikati mwambuga kubwa huko Kansas na mjombake Henry aliyekuwa mkulima, pamoja naye shangaziye Em aliyekuwa mkewe mkulima. Nyumba yao ilikuwa ndogo,kwa sababu mbao zilizotumiwa kuitengeneza ilibidi zibebwe maili nyingi. Kulikuwa na kuta nne, sakafu na paa, zilizounda chumba kimoja; chumba hiki kilikuwa na jiko iliyokuwa imejaa kutu, kabati palipowekwa sahani, meza, viti vitatu au vinne, na vitanda. Mjomba Henri na shangazi Em walikuwa na jitanda kona moja, naye Dorothy kijitanda kona nyingine. Hapakuwa na $$$$ hata, pia hapakuwa na $$$ isipokuwa shimo ndogo iliyochimbwa ardhini, iliyoitwa $$$ ya kimbuga, mahali ambapo familia ingekimbia kama mojawapo wa upepo mkubwa ungezuka , iliyokuako kubwa kubwa kiasi cha kuvunja na kuharibu nyumba yoyote pahali popote ilipopita. Ili uingie $$$ ya limbuga ulifungua mlango mdogo katikati mwa sakafu, ambapo palikuwa na ngazi iliyoshuka mpaka ndani mwa shimo hii ndogo iliyokuwa na giza. Dorothy ali

SURA YA KWANZA HADI YA TATU.

Utangulizi     Ngano. masimulizi, hekaya na hadithi nyingine zimekuwa za utotoni tangu jadi. Kila mtoto mdogo mwenye afya anazipenda kwa moyo wake wote hadithi hizi kuhusu mambo ya ajabu. Fari zenye bawa, zilizobuniwa nao Grimm na Andersen, zimeleta furaha tele katika mioyo ya watoto kuliko hadithi zote alizobuni mwanadamu.     Lakini hadithi hizi zinazohusu fari, zilizohudumuia vizazi sasa zinaweza kuwekwa katika sehemu ya vitabu vya ‘kihistoria’ katika maktaba ya watoto; wakati umefika kwa hadithi mpya za ajabu nazo zile zilizoeleka za jini,dwafu na fari kuondolewa, pamoja na mambo yote ya kutisha yaliyowekwa na watungaji hadithi ili kutoa funzo. Elimu ya kisasa inawapa watoto maadili; kwa hivyo mtoto wa kisasa anahitaji tu burudani katika hadithi zake. Mtoto huyu anatupilia mbali kwa furaha vitukio vyote asivyokubaliana navyo.     Tukiwa na fikra hizi akilini, hadithi ya “ Mganga Ajabu wa Au” iliandikwa kwa lengo moja tu la kuwafurahisha watoto wa siku hii. Hadithi hii inalenga kuwa