Skip to main content

SURA YA KWANZA HADI YA TATU.

Utangulizi
    Ngano. masimulizi, hekaya na hadithi nyingine zimekuwa za utotoni tangu jadi. Kila mtoto mdogo mwenye afya anazipenda kwa moyo wake wote hadithi hizi kuhusu mambo ya ajabu. Fari zenye bawa, zilizobuniwa nao Grimm na Andersen, zimeleta furaha tele katika mioyo ya watoto kuliko hadithi zote alizobuni mwanadamu.
    Lakini hadithi hizi zinazohusu fari, zilizohudumuia vizazi sasa zinaweza kuwekwa katika sehemu ya vitabu vya ‘kihistoria’ katika maktaba ya watoto; wakati umefika kwa hadithi mpya za ajabu nazo zile zilizoeleka za jini,dwafu na fari kuondolewa, pamoja na mambo yote ya kutisha yaliyowekwa na watungaji hadithi ili kutoa funzo. Elimu ya kisasa inawapa watoto maadili; kwa hivyo mtoto wa kisasa anahitaji tu burudani katika hadithi zake. Mtoto huyu anatupilia mbali kwa furaha vitukio vyote asivyokubaliana navyo.
    Tukiwa na fikra hizi akilini, hadithi ya “ Mganga Ajabu wa Au” iliandikwa kwa lengo moja tu la kuwafurahisha watoto wa siku hii. Hadithi hii inalenga kuwa hadithi mpya ya kisasa ambapo mambo yote ya furaha yamebakia na yale yote ya kuhuzunisha na kuhusu jinamizi yameachwa.

L. Frank Baum
Chicago, Aprili, 1900.

MGANGA AJABU WA AU

1. Kimbuga

Dorothy aliishi katikati mwa mbuga kubwa huko Kansas na mjombake Henry aliyekuwa mkulima pamoja na shangaziye Em,mkewe mkulima. Nyumba yao ilikuwa ndogo,kwa sababu mbao zilizotumiwa kuitengeneza ilibidi zibebwe maili nyingi. Kulikuwa na kuta nne, sakafu na paa, zilizounda chumba kimoja.Chumba hiki kilikuwa na jiko iliyokuwa imejaa kutu, kabati iliyowekwa sahani, meza, viti vitatu au vinne na vitanda.
Mjomba Henry na shangazi Em walikuwa na jitanda kona moja, naye Dorothy kijitanda kona nyingine. Hapakuwa na dari hata, wala gorofa ya chini isipokuwa shimo ndogo iliyochimbwa ardhini, iliyoitwa  shimo la kimbuga, mahali ambapo familia ingekimbia na kujificha kama mojawapo wa upepo mkubwa ungezuka.Upepo uliokuwa mkubwa kiasi cha kuvunja na kuharibu nyumba yoyote pahali popote ilipopita. Ili uingie shimo la kimbuga ulifungua mlango mdogo katikati mwa sakafu, ambapo palikuwa na ngazi iliyoshuka mpaka ndani ya shimo hii ndogo iliyokuwa na giza.
Dorothy aliposimama mlangoni na kutazama kila upande hakuona chochote isipokuwa mbuga kubwa yenye rangi ya kijijivu kila mahali. Kila mahali ulipotazama,  mpaka zilipokutana mbingu na ardhi, hapakuwa na mti wala nyumba. Ardhi yote iliyokuwa imetifuliwa ilikuwa imechomwa na jua na kushikamana na kuwa rangi ya kijivujivu ikiwa imepasuka pasuka.Hata nyasi nayo haikuwa rangi ya kijani, kwani ilikuwa imechomwa na jua na kuwa rangi ya kijivujivu kama ilivyokuwa ardhi. Kitambo nyumba ilikuwa imepakwa rangi, lakini jua na mvua ziliungana na kuisafisha nyumba pia ikawa rangi isiyovutia, rangi ya kijivujivu kama kila kitu kingine.
Shangazi Em alipokuja kuishi hapa alikuwa mwanamke mrembo sana. Jua na upepo zilikuwa zimembadilisha pia yeye. Macho yake yaliacha kuvutia yakawa pia rangi hii ya kijivujivu; uso wake wote ulibadilika na kuwa rangi hii mbaya. Alionekana ameishiwa na nguvu na akawa tu mifupa na aliwacha kutambasamu siku hizi. Dorothy, ambaye alikuwa ni yatima, alipokuja kuishi naye, Shangazi Em alishinda akiwika mara kwa mara Dorothy alipocheka. Mambo haya yalimshangaza sana, alishindwa mtoto huyu allikuwa akifurahishwa na nini kila wakati.
Mjombake Henry hakucheka kamwe. Alifanya kazi asubuhi mpaka usiku na hakujua furaha ilikuwa nini. Pia yeye alikuwa na rangi hii ya kijivujivu, kutoka kwa mashavu mpaka kwa viatu vyake.Alionekana mwenye fikira na huzuni na hakuzungumza sana.
Toto ndiye aliyemfanya Dorothy awe na furaha na alimzuia kubadilika rangi na kuwa kama mazingira yake. Toto hakuwa mwenye rangi ya kijivujivu; alikuwa mbwa mdogo mwenye rangi nyeusi na nywele ndefu laini kama hariri, alikuwa na macho madogo nyeusi yaliyomeremeta kila upande wa pua lake ndogo. Toto alishinda akicheza siku nzima na Dorothy alicheza naye na alimpenda sana.
Leo lakini hawakuwa wakicheza. Henry,mjombake alikaa mlangoni na kutazama mbingu akiwa na shaka kwani leo mbingu ilikuwa imebadilika na kuwa na rangi ya kujijivu kuliko kawaida. Dorothy alisimama mlangoni na kutazama  mbingu pia akiwa amemshika Toto mkononi. Em,shangaziye alikuwa akiosha sahani.
Kutoka kaskazini,kwa umbali, walisikia mlio wa upepo. Dorothy na mjombake Henry waliweza kuona nyasi ikiinama kutokana na upepo mkali uliokuwa ukivuma. Pakasikika  sauti kubwa hewani kutoka kusini, wakatazama nyuma wakaona pia nyasi ilikuwa pia ikiinama vivyo hivyo.
Ghafla Henry akasimama.
" Kimbuga cha kuja Em," alimwita mkewe. " Nitaenda kuichunga mifugo." Kisha akakimbia zizini walimoweka ngombe na farasi.
Em shangaziye akaacha kazi yake akakimbia mlangoni. Alitazama tu na akajua hatari iliyokuwa ikija.
"Dorothy kimbia!" aliwika. "Kimbia uingie kwenye Shimo la Kimbuga!"
Toto aliruka kutoka mikononi mwa Dorothy na kukimbia akajificha chini ya kitanda, naye msichana akaenda kumtafuta.Em, aliyekuwa amepatwa na mshangao mkubwa, alilifungua lango lilokuwa sakafuni na kushuka kwa ngazi mpaka ndani ya shimo iliyokuwa na giza. 
Dorothy hatimaye aliweza kumshika mbwa wake Toto na akaanza kumfuata shangaziye. Alipokuwa ametembea na kufika nusu ya chumba pakawa na kilio kikubwa cha upepo,nalo nyumba nzima likatingizika kwa kishindo mpaka Dorothy akateleza na kuanguka na kukaa kwa ghafla sakafuni. Kisha kitu cha kustaajabisha kikafanyika. Nyumba ikazunguka mara mbili tatu na ikaanza kupaa hewani. Dorothy akajihisi kama alikuwa akipaa ndani ya puto. Zilipokutana pepo kutoka kaskazini na kusini ndipo nyumba ilipokuwa imesimama na hapa pakawa katikati mwa kimbuga. Ndani katikati mwa kimbuga huwa pametulia, lakini uzito na nguvu ya upepo uliokuwa pande zote za nyumba uliibeba nyumba juu mpaka ikafika juu ya kimbuga; na hapo ikabaki na ikabebwa kilomita nyingi kwa urahisi kama nyoya.
Palikuwa na giza , upepo ulivuma kwa ukali pande zake zote, lakini Dorothy aliona ya kuwa aliweza kupaa kwa urahisi.Baada ya muda wa kwanza juu hewani, kuzungushwa na upepo na mara nyingine moja nyumba ilipopinduka vibaya, alihisi kama mtoto mchanga anavyobembelezwa  kitandani. Toto hakuipendelea hataa. Alishinda akikimbia, mara hako hapa mara ako pale kote chumbani, akibweka kwa nguvu; lakini Dorothy alikaa chini amenyamaza kimya kwenye sakafu akitarajia kitakachofanyika.
Wakati mmoja Toto alikaribia palipokuwa na shimo sakafuni, penye lango, na kuanguka ndani; Dorothy akadhani amempoteza. Lakini baada ya muda mfupi aliliona sikio moja lake likichomoza kutoka kwa shimo, nguvu ya upepo ilimzuia kuanguka kwani ilimpuliza juu. Dorothy alitambaa mpaka shimoni na kumshika Toto kwa sikio na kumvuta ndani ya chumba kisha akalifunga lango kuzuia ajali nyingine kufanyika.
Masaa ikapita, na baada ya muda Dorothy aliwacha kuogopa.Lakini alipatwa na hisia za upweke. Sauti kubwa ya upepo ilitishia kumfanya kiziwi. Mwanzoni alidhani ataangushwa chini kama nyungu na kuwa vipande nyumba ilipoanguka chini tena; lakini masaa yalipozidi kupita na hakuna lolote  mbaya lililomfanyikia, aliwacha kuwa na masikitiko na akaamua kungoja kama ametulia  na kungoja yatakayokuja. Mwishowe alitambaa juu ya sakafu iliyokuwa ikitingizika mpaka kitandani na akalala juu yake naye Toto alimfuata na kulala kando yake. Hata ingawa nyumba ilikuwa ikitingizika na upepo ulivuma kwa kelele baada ya muda Dorothy alifunga macho yake na akalala usingizi mnono.

2. Kongamano  la Dorothy na Wanyama.
Aliamshwa na kishindo kikubwa na kama Dorothy asingalikuwa amelala kitandani,angeumia.Kishindo hicho kilimfanya astaajabu na kufikiri kilichofanyika; naye Toto akaliweka pua lake baridi usoni mwa Dorothy na kutoa sauti ya hofu. Dorothy aliamka na akangalia kila mahali.Nyumba ilikuwa imewacha kusonga; na pia sasa hapakuwa na giza, kwani jua lilikuwa likiwaka kupitia kioo na kujaza chumba chote. Dorothy alitoka kitandani, akakimbia na kufungua mlango Toto akiwa anamfuata nyuma.
Msichana huyo mdogo aliwika kwa furaha kwa sababu ya mambo yote ya ajabu aliyoyaona.Macho yake yalipanuka yakawa kubwa kama sahani.
Kimbuga  kilikuwa kimetua nyumba kwa utulivu na kuiweka katika nchi ya urembo tele. Palikuwa na nyasi yenye rangi ya kijani kibichi nayo miti ilikuwa kubwa na iliyokuwa na matunda  makubwa yaliyoonekana tamu sana.Kulikuwa na maua chungu nzima kila mahali alipotazama, ndege wenye rangi ambazo akuwahi kuona maisha yake yote,wenye urembo wa kupindukia wakiwa wametua mitini. Kwa mbali kidogo kulikuwa na mto mdogo, uliokuwa ukipita katikati ya mimea ilyokuwa pande zote zake, sauti yake ilimfurahisha sana Dorothy kwani alikuwa ameishi nchi kavu miaka mingi sana.
Alipokuwa amesimama akitazama urembo huu wote, aliuona umati wa watu ukija upande wake. Walikuwa watu wa kushangaza ambao hakuwa amewaona maisha yake yote. Hawakuwa wakubwa kama watu wengine ambao alikuwa amewazoea na pia hawakuwa wafupi. Kwa uhakika walikuwa warefu kama Dorothy mwenyewe, ingawa Dorothy alikuwa mrefu kuliko umri wake, hawa walionekana wazee sana.
Watatu walikuwa wanaume na mmoja alikuwa mwanamke na wote walikuwa wamevaa mavazi yasiyo ya kawaida. Walivaa kofia duara zilizoinuka kama futi moja juu ya vichwa vyao kama pia na kengele ndogo ndogo katika mviringo wa kofia hizo ambazo zilitoa sauti nzuri sana walipotembea. Kofia za wanaume zilikuwa rangi ya buluu nayo ya mwanamke ilikuwa nyeupe na alivaa gauni nyeupe iliyokuwa na plaiti kutoka mabegani. Juu yake kulikuwa na nyota ndogo zilizometameta kwenye jua kama almasi. Wanaume walikuwa wamevalia nguo za rangi ya buluu kama kofia zao.Dorothy alifikiri wanaume hao walikuwa wenye umri moja na mjombake Henry, kwani wawili wao walikuwa na ndevu. Lakini mwanamke mdogo alikuwa mzee kuwaliko.Usoni alionekana mzee sana na nywele yake ilikuwa imejaa mvi na alitembea kwa matatizo.
Watu hawa walipokaribia nyumba aliyokuwa amesimama Dorothy, walisimama na wakaanza kuzungumza wenyewe kwa wenyewe, wakionekana wakiogopa kukaribia. Lakini mwanamke mfupi alisonga mbele na kumkaribia Dorothy na kumwinamia na akazungumza kwa sauti nzuri laini:
"Umekaribishwa ewe mganga mzuri katika nchi ya Munchkini.Tuna kushukuru sana ewe mganga mwema kwani umemuua Mchawi Mwovu kutoka mashariki, na kuokoa na kutuachilia huru kutoka utumwa wake."
Dorothy alisikiza hotuba hii kwa mshangao. Mwanamke huyu mfupi anamaanisha nini akiimwita mganga, na kusema ya kuwa aliimua Mchawi Mwovu kutoka masharikii? Dorothy alikuwa msichana mdogo tu.Ingekuaje mwanamke huyu akamwita mganga na mwenye nguvu ya kumuua mchawi.Dorothy alijipata tu amabebwa na kimbuga kilomita nyingi kutoka nyumbani; na hakuwa amewahi kuua chochote maisha yake yote.
Lakini mwanamke huyu alionekana akitarajia jibu kutoka kwake; basi Dorothy akasema bila wasiwasi," Wewe ni mkarimu sana , lakini sikuelewi unasema nini. Mimi sijamuua yeyote."
"Lakini nyumba yako imefanya hivyo," alisema mwanamke mfupi mzee kwa kicheko," na mambo hayo ni sawa. au unaonaje wewe!' aliendelea kusema akimwonyesha Dorothy kona moja ya nyumba." Unaona miguu miwili ikichomoza kutoka chini ya mbao za nyumba."
Dorothy aliangalia na kutokwa na kilio cha mshangao. Hapo, kwa uhakika, chini ya nyumba miguu miwili ilionekana ikichomoka, ikiwa imevalia viatu vya rangi ya fedha.
"Ah! Ah!," alilia Dorothy akiishika mikono kwa mshangao. "Nyumba imemwangukia tutafanya nini?"
"Hakuna chochote cha kufanya ," alisema mwanamke kwa upole.
"Lakini alikuwa nani?" aliuliza Dorothy kwa masikitiko. "Alikuwa mchawi mwovu kutoka mashariki," alimjibu mwanamke mfupi."Mwanamke huyu mwovu alikuwa amewaweka Munchkini katika maisha ya ufungwa kwa miaka mingi na kuwafanya watumwa wake usiku na mchana. Sasa wamewachiliwa huru kwa hisani yako na wanakushukuru wewe.
"Hawa Munchkini ni akina nani?" Dorothy aliuliza.
"Ni watu wanaoishi katika nchi hii ya mashariki alipotawala mwanamke mlozi."
"Je wewe ni mmoja wa Munchkini?" Dorothy aliuliza.
"La , lakini mimi ni rafiki yao, ingawa naishi katika nchi ya kaskazini.
Walipogundua ya kuwa mchawi wa mashariki amekufa ,Muchkini walituma ujumbe uje kwangu nami nikaja mara moja.Mimi ni mganga kutoka kaskazini.
"Ah!" alilia Dorothy. "Wewe pia ni mchawi?"
"La hasha ," alimjibu mwanamke mfupi."Mimi ni mganga mwema anayependwa na watu. Mimi sina nguvu nyingi kama alizokuwa nazo mchawi mwovu aliyetawala , au nami ningeweza kuwakomboa watu kwa nguvu zangu."
"Lakini nilidhani yakuwa wachawi wote ni wabaya ," alisema msichana ambaye alikuwa akiogopa kumwona mchawi wa kweli."Ndiyo huo ni ukweli . Kuna waganga na wachawi. Huku nchi ya Au kuna waganga wawili wanaoishi kusini na kaskazini, hao ni wale wazuri. Huo ni ukweli kwani mimi ndiye mmoja wao na haiwezi kuwa nimekosea.
Wale wanaoishi mashariki na magharibi ni waovu kabisa , wanawake wawili wachawi; lakini sasa kwa kuwa umemuua mmoja , kunaye tu mchawi mmoja mwovu nchi ya Au, yule anayeishi magharibi."
"Lakini," alisema Dorothy, baada ya kufikiri kwa muda." Shangazi yangu Em ameniambia ya kuwa wachawi wote walikufa karne nyingi zilizopita."
"Ni nani huyu shangazi Em?" aliuliza mwanamke huyo mdogo mzee.
"Yeye ni shangazi yangu anayeishi Kansas nilipotoka."
Mganga kutoka kaskazini alionekana akifikiri kwa muda akiwa ameinamisha kichwa chake na macho yake chini. Kisha akaangalia juu akasema, " Sijui huko Kansas ni wapi, kwani sijawahi kukusikia . Je huko utokako ni nchi yenye ustaarabu.
"Ndio," alimjibu Dorothy.
"Basi ndio kwa maana . Huko katika nchi za ustaarabu hakuna waganga, wachawi, wahini na hata walozi. Lakini hapa nchi ya Au, hatujawahi kupata ustarabu, kwani tumefungiwa kutoka nchi zingine za ulimwengu. Hiyo ndio sababu tunao bado waganga na wachawi"
"Mnao waganga wanaume?"
"Au mwenyewe ndiye mganga mwenye nguvu sana." alimjibu mwanamke  mfupi huku akinuninong'oneza sauti." Yeye ana nguvu kutuliko sisi sote naye anaishi katika Jiji la Zumaridi."
Dorothy alikuwa karibu kuuliza swali lingine , lakini Munchkini waliokuwa wamesima wametulia tuli ghafla walipiga kelele wakiwa wanaashiria kwa kidole kona moja ya nyumba alipokuwa amelala mchawi mwovu aliyekufa.
"Ni nini?" aliuliza mwanamke mdogo mzee huku akitazama. Baada ya kuona kilichowashangaza Munchkini alitoa kicheko.Miguu ya mchawi mwovu ilikuwa imepotea na kuacha tu jivu na viatu vyake vya rangi ya fedha.
"Alikuwa ameezeeka sana," alielezea mganga kutoka magharibi," Mpaka akakauka chini ya jua kali mpaka akawa tu jivu na mchanga. Huo ndio mwisho wake. Lakini viatu vyake vya fedha ni vyako na utavichukua uvalie." Aliinama chini na kuvichukua , baada ya kupanguza vumbi alimpa Dorothy.
"Mchawi kutoka mashariki alivipenda sana viatu hivi vya fedha," alisema mmoja wa munchkini. ''Na pia tumesikia ya kuwa kuna uchawi unaoandamana na viatu hivyo; lakini hatukuweza kujua ni nini."
Dorothy alivibeba viatu mpaka ndani ya nyumba na kuviweka juu ya meza. Akarudi tena kwa Munchkini akasema: " Ningetaka sana kurudi kwa shangazi yangu na mjomba wangu, kwa sababu nina uhakika wakonawasiwasi juu hali yangu, je unaweza kunisaidia kupata njia?”
Muchkini na mganga waliangaliana halafu wakamtazama Dorothy kisha wakatikisa vichwa vyao.
"Mashariki, mbali kidogo na hapa," alisema mmoja. ''kuna jangwa kubwa na hakuna anayeweza kulipita akiwa hai.''
"Kusini pia shida ni hiyo hiyo," alisema mmoja," kwani, nimeshawahi kwenda huko na kuona. Kusini ni nchi ya wanyama wanaoitwa Kadili."
"Niliambiwa," alisema wa tatu,"Magharibi pia mambo ni hayo tu. Nchi hiyo ndiyo wanyama waitwao Winki wanamoishi. ''Huko ndiko anakotawala mchawi mwovu wa magharibi, ambaye humfanya mtumwa yeyote apitaye upande huo.
Kaskazini ni nyumbani kwangu," alisema mwanamke mkongwe, " pia huko kumezungukwa na jangwa kama ilivyo nchi yote ya Au. Nina hofia mwanangu itabidi uishi nasi."
Baada ya kusikia haya alianza kulia kwa majonzi, kwa sababu alianza kupatwa na hisia za upweke kwani alikuwa mbali sana kutoka nyumbani na watu hawa asiowajua. Kilio chake kiliwahuzunisha Munchkini waliokuwa na moyo mkarimu.Wao pia walitoa vitambaa na wakaanza pia kulia. Mwanamke mzee alitoa kofia yake na akaiweka puani na akaanza kuhesabu," Moja, mbili, tatu" na sauti ya huzuni. Mara tu kofia hiyo ikabadilika na kuwa ubao mdogo uliokuwa umeandikwa kwa chaki nyeupe ujumbe huu:
"Wacheni Dorothy aende jiji la Zumaride."
Mwanamke mzee mdogo alilitoa ubao kutoka puani na baada ya kuyasoma maneno, aliuliza, " Jina lako ni Dorothy ewe mwanangu?"
"Ndio," alijibu mtoto, huku akipanguza machozi yake.
"Basi ni lazima uende katika jiji la Zumaride.Pengine mganga Au atakusaidia."
"Liwapi jiji hili?'' aliuliza Dorothy.
"Lipo katika nchi inayotawaliwa na Au mwenyewe mganga niliyekuelezea juu yake.
"Je, yeye ni mtu mwema?" aliuliza msichana kwa huzuni.
"Yeye ni mganga mwema. Kama yeye ni mwanamume au mwanamke mimi sijui, kwani sijawahi kumwona."
"Nitafika vipi kwake?" aliuliza Dorothy.
"Itakubidi utembee.Ni njia ndefu inayopitia nchi ambayo wakati mwingine ni nzuri na yenye giza na mabaya. Lakini nitatumia uganga wangu wote kukulinda kutoka mabaya.
"Utaandamana nami?" aliomba msichana, ambaye kwa sasa alianza kumwona mwanamke huyu mzee kama rafiki yake.
"La siwezi," alimjibu, ''Lakini nitakupa busu langu, na hakuna yeyote anayejaribu kumdhuru aliye na busu la mganga wa magharibi.
Alikaribia na kumbusu Dorothy kwenye kipaji cha uso. Alipomguza msichana paliwachwa na alama iliyokuwa ikingaa.Dorothy aliigundua hivyo baada ya haya.
''Barabara ya kuelekea jiji la Zumaride limejengwa kwa mawe ya rangi ya manjano,'' alisema mganga."Hivyo basi huwezi kupotea. Utakapofika kwake Au usimwogope, mweleze yaliyokufanyikia an umwombe msaada.Kwaheri mwanangu mpendwa,"
Muchkini watatu walimwinamia na wakamtakia safari njema, na baada ya hayo walienda zao kupitia upande wa miti. Mganga alimpungia mkono, akazunguka mara tatu, ghafla akapotelea hakuonekana tena.Toto alishangazwa sana na kupotea kwa mganga huyu.Toto alibweka sana kwani alikuwa amemuogopa sana mganga alipokuwa amesima karibu.
Lakini Dorothy, kwa sababu alijua ya kuwa alikuwa mganga alitarajia aondoke vivyo hivyo na hakushangazwa hata kidogo.

3. Jinsi Dorothy Alivyomuokoa Kifukuzakunguru
Dorothy alipoachwa peke yake alianza kuhisi njaa. Basi akaenda kabatini akajikatia kipande cha mkate kisha akapaka siagi. Alimpa Toto pia mkate, akachukua ndoo na akaenda mtoni kuteka maji. Toto alikimbia mitini ambapo aliwaona ndege na akaanza kuwabwekea. Dorothy alimfuata na hapo mitini aliweza kuona matunda matamu ambayo alichukua kidogo ili ale kama staftahi.
Akarudi tena kwenye nyumba na baada ya kutuliza kiu kwa maji matamu ya mto alianza kupanga safari yake ya kuelekea Jiji la Zumaride.
Dorothy alikuwa na rinda moja nyingine tu lakini hilo lilikuwa safi na lilikuwa limeanikwa kwenye msumari kando ya kitanda chake. Nalo hili lilikuwa la madoadoa ya rangi ya samawati na nyeupe. Lakini rangi ya buluu ilikuwa imepungua umaridadi wake baada ya kuoshwa mara nyingi, lakini bado ilikuwa nguo nzuri sana. Msichana alinawa kwa uangalifu na kuivalia nguo hio ya bafia yenye madoafoa.Akavalia kofia yake ya kujikinga kutokana na jua iliyokuwa rangi ya waridi. Akachukua kijikapu akajaza mkate kutoka kwa kabati kisha akafunika kwa kitambaa cheupe juu. Alipoangalia viatu vyake aliona ya kuwa vilikuwa vimezeeka na kuchakaa.
" Hivi viatu kweli havitafaa kwa safari ndefu." Dorothy alimwambia Toto. Toto alimwangalia usoni Dorothy kwa macho yake meusi akatingiza mkia wake kumuashiria ya kuwa alielewa alichokua akimaanisha.
Hapo basi Dorothy alitazama na kuona viatu vya fedha vilivyokuwa vya mchawi wa mashariki.
"Vyaweza kunitosha kweli,'' alimwambia Toto." Viatu hivi vinafaa kweli kwa safari ndefu kwa sababu haviwezi kuharibika.
Alivitoa viatu vyake vilivyokuwa vimezeeka na kuvalia viatu hivyo vya fedha ambavyo vilimtosha vizuri; kana kwamba vilitengenezewa yeye tu.
Mwishowe akachukua kikapu chake. " Hebu kuja Toto," alisema," Tutakwenda Jiji la Zumaridi na kumuuliza Au,mganga mkuu, tutakavyorudi Kansas tena."
Alifunga mlango kwa kifunguo na kukiweka kifunguo mfukoni mwa rinda lake. Akaanza safari yake, Toto akifuatilia kwa mwendo wa aste aste.
Kulikuwako na barabara nyingi alizoziona lakini ilimchukua muda mfupi na hatimaye aliweza kuipata barabara iliyokuwa imetengenezwa na matofali ya rangi ya manjano. Safari yake ikaanza rasmi akaanza kuifuata barabara akielekea Jiji la Zumaridi, viatu vyake vya fedha vikitoa sauti nzuri alipotembea barabarani.
Ndege waliimba kila mahali kwa sauti nzuri huku jua likiwa limewaka kwa nguvu. Dorothy hakuwa na masikitiko kama unavyodhani msichana mdogo angehisi baada ya kubebwa na kimbuga na kuwekwa katika nchi asiyoifahamu.
Alipokuwa akitembea alishangazwa kuona nchi ilivyokuwa maridadi kila mahali alipotazama.Kando ya barabara kulikuweko na sera maridadi iliyokuwa imepakwa rangi ya buluu.Kwa umbali aliona shamba zilikuwa na mazao mazuri ya nafaka mbali mbali na pia aina nyingi za mboga. Munchkini walikuwa wakulima hodari sana.
Mara kwa mara alipopita kando ya nyumba ya mmojawapo wa Munchkini,wenyeji walitoka na kumuinamia kwa sababu walijua ni kwa sababu yake mchawi mwovu wa mashariki aliuawa na kuwakomboa watu wote. Nyumba walizoishi Munchkini zilikuwa za kushangaza mno. Muundo wake ulikuwa wa duara, paa lilifanana kama nusu tanga. Nyumba zote zilikuwa zimepakwa rangi ya samawati.
Ilipofika jioni Dorothy alianza kuwa na uchovu mwingi baada ya kutembea kwa muda mrefu. Dorothy alianza kuwaza atakapolala usiku uingiapo. Alifika kwenye nyumba moja iliyokuwa kubwa kuliko zingine. Nje ya nyumba hiyo kulikuwa na wanaume na wanawake waliokuwa wakicheza densi.Wanamuziki walionekana wakicheza muziki kwa ushupavu na walipaaza sauti sana.Pia karibu nao Dorothy aliliona jimeza lilokuwa limejaa matunda, punje, mikate, keki na vitu vingi kochokocho vya kula.
Watu hawa walimkaribisha Dorothy kwa moyo mkunjufu aje ale nao na apate mahala pa kulala usiku huo.Nyumba hii ilikuwa ya Munchkini tajiri sana nchi yote, na alikuwa amewakaribisha marafiki wake waje kwa sherehe ya kuachiliwa huru kwao kutoka kwa mchawi mwovu.
Dorothy alikula na akashiba sana. Mwenye nyumba alimpakulia kile alichotaka yeye mwenyewe.Jina la Munchkini tajiri lilikuwa Boku.Walikaaa kwenye sofa na kuwatazama watu wakicheza densi.
"Yaonekana ya kuwa wewe ni mchawi mwenye nguvu nyingi sana." Boku alisema baada ya kuviona viatu vyake Dorothy vyenye rangi ya fedha.
"Mbona wasema hivyo?" aliuliza msichana.
"Kwa sababu una viatu vya fedha na ulimuua mchawi mwovu.Halikadhalika nguo yako ni nyeupe na ni wachawi peke yake huvaa nguo nyeupe."
"Nguo yangu ni buluu na ina madoadoa meupe," alisema Dorothy,huku akinyorosha nguo lake.
"Umefanya vyema kuvalia hivyo," alisema Boku."Buluu ni rangi ya Munchkini na nyeupe ni rangi ya wachawi.Basi tunajua wewe ni mchawi mwema."
Dorothy alishindwa asememe nini.Yeye alijua ya kuwa hakuwa mchawi alikuwa tu msichana aliyebebwa na kimbuga kutoka mbali na kuletwa hapa hata ingawa watu wote walimdhania kuwa mchawi.
Baada ya kuchoka kutazama densi,mwenye nyumba alimwonyesha chumba chake cha kulala.Chumba hiki kilikuwa na kitanda maridadi mno.Matandiko yalikuwa ya rangi ya buluu.Dorothy alilala fofofo.Toto alilala kwenye mkeka uliokuwa wenye rangi ya buluu kando ya kitanda chake Dorothy.
Dorothy alikula kiamsha kinywa kikubwa.Baadaye alimuona mtoto mchanga Munchkini,aliyekuwa akicheza na Toto.Mtoto huyu alimchekesha sana Dorothy alivyovuta mkia wake Toto na ucheshi wake.Watu hawa walimchunguza sana Toto kwa sababu hawakuwa wamewahi kumuona mbwa.
"Jiji la Zumaridi liko umbali gani?" alimuuliza msichana.
''Sijui mimi," alimjibu Dorothy kwa kuogopa."Sijawahi kwenda huko.Watu wameonelea kutomkaribia Au isipokuwa kama una mambo muhimu naye.Njia ya kuelekea Jiji la Zumaridi ni ndefu na itakuchukua siku nyingi kufika.Nchi unayopita kwa sasa ni nzuri lakini utapita penye hatari huko mbele kabla ufike mwisho wa safari yako."
Jambo hili lilimsikitisha Dorothy kidogo, lakini alijua tu ni Au aliyeweza kumsaidia.Basi akaamua kwa ushujaa kuendelea na kutorudi nyuma.
Aliwaaga marafiki wake na kuuanza safari yake kwenye njia ya matofali yenye rangi ya manjano.Baada ya kutembea maili kadha aliona apumzike basi akapanda juu ya sera na kuketi chini.Kulikuwa na shamba la mahindi kubwa mbali kidogo na sera.Kwa umbali aliliona Kifukuzakunguru, lilokuwa limewekwa juu kwa kijiti kirefu kufukuza ndege wasile mahindi yaliokuwa yameiva.
Dorothy alilitazama Kifukuzakunguru kwa mawazo akilini.Kichwa chake kilikuwa kimetengenezwa kwa gunia lililojazwa nyasi, macho yake, pua, na mdomo yalikuwa yamechorwa kwa rangi kuonyesha sura yake.Kofia kukuu, iliyokuwa na muumbo wa pia, ya rangi ya buluu, kama ya munchkini ilikuwa imewekwa kichwani mwake.Mwili wake wote uliokuwa na nguo za rangi ya buluu ulikuwa umejazwa nyasi.Kwenye miguu yake alivalishwa viatu vilivyokuwa vimechakaa vya rangi ya buluu kama alivyoviona na Munchkini wengine nchini kwote.Kitu hiki kilikuwa kimeinuliwa juu, juu ya mimea ya mahindi kwa kijiti kirefu kilichokuwa kimewekwa mgongoni mwake.
Dorothy alipokuwa akiitizama uso wa kifukuzakunguru uliokuwa umepakwa rangi alishangazwa kuona jicho lake moja likimkonyezea.Alidhani pengine alikuwa amekosea mwanzoni, kwa sababu nyumbani Kansas vifukuza kunguru kweli hawajawahi kukonyeza macho. Kitu hiki sasa likaanza kutingiza kichwa chake kwa kumuita.Akashuka kutoka kwenye sera na kuanza kutembea kuelekea upande wake.Toto alikimbia na kukizunguka zunguka kijiti huku akibweka.
"Hujambo," alisema Kifukuzakunguru, kwa sauti yenye ambayo haikuwa laini.
"Umezungumza"? aliuliza msichana, kwa mshangao.
"Ndio," alimjibu Kifukuzakunguru. "Hujambo?"
"Sijambo, ahsante," Dorothy alijibu kwa heshima. "Hujambo ?"
"Nina maumivu," alisema Kifukuzakunguru kwa tabasamu."Nimechoshwa sana kukaa hapa usiku na mchana kuwafukuza kunguru."
"Huwezi shuka?" aliuliza Dorothy.
"Hapana kwani kijiti hiki kimewekwa mgongoni mwangu na hakiwezi kutoka.Kama unaweza kukitoa nitakushukuru sana."
Dorothy aliinua mikono yake na kukitoa Kifukuzakunguru kutoka kwa kijiti hicho.Hakikuwa na uzito kwani kilikuwa kimejazwa nyasi tu.
"Ashanti sana," alisema Kifukuzakunguru alipowekwa chini. "Najisikia kama mtu mpya"
Dorothy alishangazwa sana na haya aliyoyaona kwa sababu hakuterejea kumuona mtu aliyekuwa amejazwa nyasi, akizungumza, akiona, akimwinamia na akitembea kando yake.
"Wewe ni nani?" aliuliza Kifukuzakunguru baada ya kujinyoosha."Na waelekea wapi?"
"Jina langu ni Dorothy," alisema Dorothy."Naelekea Jiji la zumaridi kumuomba Au Mkuu anirudishe Kansas."
"Jiji la Zumaride liko wapi?" aliuliza. "Na Au ni nani?"
"Kwani humjui? aliuliza kwa mshangao.
"Kwa uhakika la.Sijui chochote.Unaona mimi nimejazwa tu nyasi sina akili hata," alisema kwa huzuni.
"Ooo!" alisema Dorothy."Pole sana"
"Unadhani ," aliuliza, "Nikienda Jiji la Zumaridi na wewe, kuwa Au atanipa akili?"
"Siwezi kujua," alisema, "Lakini waweza kuja nami ukipenda.Ikiwa Au atakupa akili au hatakupa hutakuwa umepoteza chochote."
"Huo ni ukweli,"alisema."Wajua," aliendelea,"sijali ikiwa miguu yangu na mwili umejazwa nyasi, kwa sababu siwezi umia.Yeyote akinikanyaga kwa mguu au kunidunga kwa pini haijalishi kwa sababu sitaihisi.Lakini sitaki watu waniite mpumbavu.Kichwa changu kikiwa kimejazwa nyasi badala ya akili kama lako nitawezaje kujua chochote?"
"Naelewa unayosema," alisema msichana akimwonea huruma sana. "Ukiandamana nami nitamwomba Au akufanyie yote awezayo."
"Ahsante," alijibu kwa shukrani.
Walirudi barabarani.Dorothy alimsaidia kuruka sera na wakaanza safari yao kwenye njia ya matofali yenye rangi ya manjano wakielekea Jiji la Zumaridi.
Toto hakupendezwa na huyu mgeni mpya.Alinusanusa kana kwamba kulikuwa na panya ndani yake kwenye nyasi na mara kwa mara alimgurumia Kifukuzakunguru.
"Usimjali Toto," alimwambia Dorothy rafiki wake mpya. "Hawezi kuuma."
"Mimi siogopi," alimjibu Kifukuzakunguru."Hawezi kuiumiza nyasi.Wacha nikubebee kapu lako.Haitakuwa mzingo kwa sababu sichoki.''Nikuambie siri," aliendelea, akitembea.
"Kuna kitu moja tu duniani ambalo mimi huogopa."
"Na ni nini hicho?" aliuliza Dorothy."Mkulima Munchkini aliyekuumba?"
"La," alijibu Kifikuzakunguru. "Kiberiti kilichowashwa."

Comments

Popular posts from this blog

Swahili translation of the Wonderful Wizard of Oz

Hii ni tafsiri ya kitabu cha L. Frank Baum, The Wonderful Wizard of Oz. Jina lake baada ya kufikiri na kuchunguza maana ya Oz nimeona katika kiswahili ,"Mganga Ajabu Wa Au." Oz lilitokana na ufupisho wa neno Ounce  ambacho ni kipimo cha dhahabu, Kwa ksiwahili ni Aunsi nami nikafupisha likawa Au, ambayo imenipa Mganga Au. I will publish a chapter by chapter of the whole book. Copyright 2011

Mganga Ajabu Wa Au, sura ya kwanza

MGANGA AJABU WA AU 1. Kimbuga Dorothy aliishi katikati mwambuga kubwa huko Kansas na mjombake Henry aliyekuwa mkulima, pamoja naye shangaziye Em aliyekuwa mkewe mkulima. Nyumba yao ilikuwa ndogo,kwa sababu mbao zilizotumiwa kuitengeneza ilibidi zibebwe maili nyingi. Kulikuwa na kuta nne, sakafu na paa, zilizounda chumba kimoja; chumba hiki kilikuwa na jiko iliyokuwa imejaa kutu, kabati palipowekwa sahani, meza, viti vitatu au vinne, na vitanda. Mjomba Henri na shangazi Em walikuwa na jitanda kona moja, naye Dorothy kijitanda kona nyingine. Hapakuwa na $$$$ hata, pia hapakuwa na $$$ isipokuwa shimo ndogo iliyochimbwa ardhini, iliyoitwa $$$ ya kimbuga, mahali ambapo familia ingekimbia kama mojawapo wa upepo mkubwa ungezuka , iliyokuako kubwa kubwa kiasi cha kuvunja na kuharibu nyumba yoyote pahali popote ilipopita. Ili uingie $$$ ya limbuga ulifungua mlango mdogo katikati mwa sakafu, ambapo palikuwa na ngazi iliyoshuka mpaka ndani mwa shimo hii ndogo iliyokuwa na giza. Dorothy ali