Skip to main content

Mganga Ajabu Wa Au, sura ya kwanza

MGANGA AJABU WA AU

1. Kimbuga

Dorothy aliishi katikati mwa mbuga kubwa huko Kansas na mjombake Henry aliyekuwa mkulima pamoja na shangaziye Em, mkewe mkulima. Nyumba yao ilikuwa ndogo, kwa sababu mbao zilizotumika kuijenga ilibidi zibebwe kilomita nyingi. Kulikuwa na kuta nne, sakafu na paa, zilizounda chumba kimoja. Chumba hiki kilikuwa na jiko iliyokuwa imejaa kutu, kabati iliyowekwa sahani, meza, viti vitatu au vinne na vitanda.

Mjomba Henry na shangazi Em walikuwa na jitanda kona moja, naye Dorothy kijitanda kona nyingine. Hapakuwa na dari hata, wala gorofa ya chini isipokuwa shimo ndogo iliyochimbwa ardhini, iliyoitwa  shimo la kimbuga, mahali ambapo familia ingekimbia na kujificha kama mojawapo wa upepo mkubwa ungezuka.Upepo uliokuwa mkubwa kiasi cha kuvunja na kuharibu nyumba yoyote pahali popote ilipopita. Ili uingie shimo la kimbuga ulifungua mlango mdogo katikati mwa sakafu, ambapo palikuwa na ngazi iliyoshuka mpaka ndani ya shimo hii ndogo iliyokuwa na giza.

Dorothy aliposimama mlangoni na kutazama kila upande hakuona chochote isipokuwa mbuga kubwa yenye rangi ya kijijivu kila mahali. Kila mahali ulipotazama,  mpaka zilipokutana mbingu na ardhi, hapakuwa na mti wala nyumba. Ardhi yote iliyokuwa imetifuliwa ilikuwa imechomwa na jua na kushikamana na kuwa rangi ya kijivujivu ikiwa imepasuka pasuka.Hata nyasi nayo haikuwa rangi ya kijani, kwani ilikuwa imechomwa na jua na kuwa rangi ya kijivujivu kama ilivyokuwa ardhi. Kitambo nyumba ilikuwa imepakwa rangi, lakini jua na mvua ziliungana na kuisafisha nyumba pia ikawa rangi isiyovutia, rangi ya kijivujivu kama kila kitu kingine.

Shangazi Em alipokuja kuishi hapa alikuwa mwanamke mrembo sana. Jua na upepo zilikuwa zimembadilisha pia yeye. Macho yake yaliacha kuvutia yakawa pia rangi hii ya kijivujivu; uso wake wote ulibadilika na kuwa rangi hii mbaya. Alionekana ameishiwa na nguvu na akawa tu mifupa na aliwacha kutambasamu siku hizi. Dorothy, ambaye alikuwa ni yatima, alipokuja kuishi naye, Shangazi Em alishinda akiwika mara kwa mara Dorothy alipocheka. Mambo haya yalimshangaza sana, alishindwa mtoto huyu allikuwa akifurahishwa na nini kila wakati.
Mjombake Henry hakucheka kamwe. Alifanya kazi asubuhi mpaka usiku na hakujua furaha ilikuwa nini. Pia yeye alikuwa na rangi hii ya kijivujivu, kutoka kwa mashavu mpaka kwa viatu vyake.Alionekana mwenye fikira na huzuni na hakuzungumza sana.

Toto ndiye aliyemfanya Dorothy awe na furaha na alimzuia kubadilika rangi na kuwa kama mazingira yake. Toto hakuwa mwenye rangi ya kijivujivu; alikuwa mbwa mdogo mwenye rangi nyeusi na nywele ndefu laini kama hariri, alikuwa na macho madogo nyeusi yaliyomeremeta kila upande wa pua lake ndogo. Toto alishinda akicheza siku nzima na Dorothy alicheza naye na alimpenda sana.
Leo lakini hawakuwa wakicheza. Henry,mjombake alikaa mlangoni na kutazama mbingu akiwa na shaka kwani leo mbingu ilikuwa imebadilika na kuwa na rangi ya kujijivu kuliko kawaida. Dorothy alisimama mlangoni na kutazama  mbingu pia akiwa amemshika Toto mkononi. Em,shangaziye alikuwa akiosha sahani.

Kutoka kaskazini,kwa umbali, walisikia mlio wa upepo. Dorothy na mjombake Henry waliweza kuona nyasi ikiinama kutokana na upepo mkali uliokuwa ukivuma. Pakasikika  sauti kubwa hewani kutoka kusini, wakatazama nyuma wakaona pia nyasi ilikuwa pia ikiinama vivyo hivyo.
Ghafla Henry akasimama.
" Kimbuga cha kuja Em," alimwita mkewe. " Nitaenda kuichunga mifugo." Kisha akakimbia zizini walimoweka ngombe na farasi.
Em shangaziye akaacha kazi yake akakimbia mlangoni. Alitazama tu na akajua hatari iliyokuwa ikija.
"Dorothy kimbia!" aliwika. "Kimbia uingie kwenye Shimo la Kimbuga!"
Toto aliruka kutoka mikononi mwa Dorothy na kukimbia akajificha chini ya kitanda, naye msichana akaenda kumtafuta.Em, aliyekuwa amepatwa na mshangao mkubwa, alilifungua lango lilokuwa sakafuni na kushuka kwa ngazi mpaka ndani ya shimo iliyokuwa na giza. 

Dorothy hatimaye aliweza kumshika mbwa wake Toto na akaanza kumfuata shangaziye. Alipokuwa ametembea na kufika nusu ya chumba pakawa na kilio kikubwa cha upepo,nalo nyumba nzima likatingizika kwa kishindo mpaka Dorothy akateleza na kuanguka na kukaa kwa ghafla sakafuni. Kisha kitu cha kustaajabisha kikafanyika. Nyumba ikazunguka mara mbili tatu na ikaanza kupaa hewani. Dorothy akajihisi kama alikuwa akipaa ndani ya puto. Zilipokutana pepo kutoka kaskazini na kusini ndipo nyumba ilipokuwa imesimama na hapa pakawa katikati mwa kimbuga. Ndani katikati mwa kimbuga huwa pametulia, lakini uzito na nguvu ya upepo uliokuwa pande zote za nyumba uliibeba nyumba juu mpaka ikafika juu ya kimbuga; na hapo ikabaki na ikabebwa kilomita nyingi kwa urahisi kama nyoya.
Palikuwa na giza , upepo ulivuma kwa ukali pande zake zote, lakini Dorothy aliona ya kuwa aliweza kupaa kwa urahisi.Baada ya muda wa kwanza juu hewani, kuzungushwa na upepo na mara nyingine moja nyumba ilipopinduka vibaya, alihisi kama mtoto mchanga anavyobembelezwa  kitandani. Toto hakuipendelea hataa. Alishinda akikimbia, mara hako hapa mara ako pale kote chumbani, akibweka kwa nguvu; lakini Dorothy alikaa chini amenyamaza kimya kwenye sakafu akitarajia kitakachofanyika.

Wakati mmoja Toto alikaribia palipokuwa na shimo sakafuni, penye lango, na kuanguka ndani; Dorothy akadhani amempoteza. Lakini baada ya muda mfupi aliliona sikio moja lake likichomoza kutoka kwa shimo, nguvu ya upepo ilimzuia kuanguka kwani ilimpuliza juu. Dorothy alitambaa mpaka shimoni na kumshika Toto kwa sikio na kumvuta ndani ya chumba kisha akalifunga lango kuzuia ajali nyingine kufanyika.

Masaa ikapita, na baada ya muda Dorothy aliwacha kuogopa.Lakini alipatwa na hisia za upweke. Sauti kubwa ya upepo ilitishia kumfanya kiziwi. Mwanzoni alidhani ataangushwa chini kama nyungu na kuwa vipande nyumba ilipoanguka chini tena; lakini masaa yalipozidi kupita na hakuna lolote  mbaya lililomfanyikia, aliwacha kuwa na masikitiko na akaamua kungoja kama ametulia  na kungoja yatakayokuja. Mwishowe alitambaa juu ya sakafu iliyokuwa ikitingizika mpaka kitandani na akalala juu yake naye Toto alimfuata na kulala kando yake. Hata ingawa nyumba ilikuwa ikitingizika na upepo ulivuma kwa kelele baada ya muda Dorothy alifunga macho yake na akalala usingizi mnono.

Comments

Popular posts from this blog

Swahili translation of the Wonderful Wizard of Oz

Hii ni tafsiri ya kitabu cha L. Frank Baum, The Wonderful Wizard of Oz. Jina lake baada ya kufikiri na kuchunguza maana ya Oz nimeona katika kiswahili ,"Mganga Ajabu Wa Au." Oz lilitokana na ufupisho wa neno Ounce  ambacho ni kipimo cha dhahabu, Kwa ksiwahili ni Aunsi nami nikafupisha likawa Au, ambayo imenipa Mganga Au. I will publish a chapter by chapter of the whole book. Copyright 2011

Mganga Ajabu Wa Au, utangulizi

Utangulizi  Ngano, masimulizi, hekaya na hadithi nyingine zimekuwa za utotoni tangu zamani, kila mtoto mdogo mwenye afya huwa na upendo kamili na wa asili kwa hadithi hizi kuhusu mambo ya ajabu na ya dhahiri kuwa si ya kweli. Fairi wenye mabawa wa Grimm na Andersen, zimeleta furaha tele katika mioyo ya kitoto kuliko kuliko viumbe vingine vyote vya wanadamu. Lakini hadithi hizi zinazohusu fairi, zilizotumika kwa vizazi, sasa zinaweza kuwekwa katika sehemu ya vitabu vya ‘kihistoria’ kwenye maktaba ya watoto; wakati umefika kwa mfululizo mpya wa  “hadithi za ajabu”  ambazo zimeodolewa dhana za jini, dwafu na fairi, pamoja na mambo yote ya kutisha na ya hofu iliyoundwa na waandishi wao kuashiria maadili ya kutishia kwa kila hadithi. Elimu ya kisasa inajumuisha maadilii; kwa hivyo mtoto wa kisasa anahitaji tu burudani katika hadithi zake za ajabu na kwa furaha huachana na matukio yote yasiyokubalika.   Tukiwa na wazo hili  akilini, hadithi ya “Mganga Ajabu wa Au” i...